Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji

Habari

DKT. CHAYA ATOA MAELEKEZO KUIMARISHA BIASHARA NA UWEKEZAJI MUFINDI


Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mheshimiwa Dkt. Pius Stephen Chaya (Mb), ameelekeza kuanzishwa kwa dawati maalum la kushughulikia kero za wawekezaji na mfumo wa huduma za pamoja (One Stop Centre) ili kurahisisha taratibu za uwekezaji nchini.

Dkt. Chaya ametoa maelekezo hayo wakati akifungua Kongamano la Biashara na Uwekezaji Mufindi 2026, lililofanyika Mafinga, mkoani Iringa, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Alexander Mkumbo.

Amesema kongamano hilo ni jukwaa muhimu la kutangaza fursa za kiuchumi, kuvutia mitaji na teknolojia, kupanua masoko na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi.

Akizungumzia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Dkt. Chaya amebainisha kuwa sekta binafsi inatarajiwa kuchangia takribani asilimia 70 ya uwekezaji nchini, akisisitiza umuhimu wa kuongeza thamani ya mazao, kukuza viwanda na kutengeneza ajira kwa vijana na wanawake.

Aidha, ameitaka Wilaya ya Mufindi kuhakikisha kongamano hilo linakuwa endelevu kwa kufuatilia makubaliano ya uwekezaji yatakayofikiwa, huku akiwahimiza wananchi kutumia fursa za mitaji na mikopo kukuza shughuli za uzalishaji na biashara.

Amewapongeza uongozi wa Wilaya ya Mufindi na wadau wote kwa kuandaa kongamano hilo, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kwa lengo la kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.