Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji

Habari

SERIKALI YAWEKA VIPAUMBELE SITA KATIKA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA WA MWAKA 2027/28


Serikali imewasilisha Bungeni Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka wa fedha 2027/28, unaolenga kuharakisha mageuzi ya kiuchumi na kijamii, kuongeza tija na ushindani wa uchumi pamoja na kuboresha ustawi wa wananchi, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP IV).

Akiwasilisha mapendekezo hayo leo tarehe 28 Oktoba, 2026, Bungeni Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, ameeleza kuwa vipaumbele sita vya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2027/28 ni kujenga uchumi imara, jumuishi na shindani; kuimarisha uwezo wa watu na maendeleo ya jamii; kuhifadhi mazingira na kuongeza ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi; kuimarisha vichocheo vya maendeleo; kuimarisha utekelezaji wa sekta za mageuzi; na kuimarisha misingi ya uendelevu wa Taifa.

Prof. Mkumbo ameongeza kuwa katika eneo la uchumi na uwekezaji, Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, kuongeza tija katika uzalishaji, kuimarisha viwanda, kurahisisha mifumo ya udhibiti na kupanua ushiriki wa sekta binafsi katika kuchochea maendeleo.

Aidha, Serikali itaweka mkazo katika kuendeleza rasilimali watu kupitia elimu yenye kuzingatia mahitaji ya soko la ajira, mafunzo ya ujuzi, sayansi na teknolojia, upatikanaji wa ajira kwa vijana, biashara ndogo na za kati pamoja na kuendelea na maandalizi ya utekelezaji wa elimu ya sekondari kwa wote kuanzia mwaka 2028 na kipaumbele kitawekwa katika kuimarisha miundombinu ya nishati, barabara, reli, bandari na viwanja vya ndege, matumizi ya teknolojia za kidijitali, uhifadhi wa mazingira, kukamilisha miradi ya umwagiliaji na kuongeza thamani ya mazao na bidhaa za viwandani.

Prof. Mkumbo amesisitiza kuwa utekelezaji wa Dira 2050 unahitaji ushirikiano wa Serikali, Bunge, sekta binafsi, mamlaka za Serikali za Mitaa, taasisi za elimu na utafiti, washirika wa maendeleo na wananchi kwa ujumla.