Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji

Habari

DKT. CHAYA AFUNGUA KONGAMANO LA TANO LA KIMATAIFA LA USIMAMIZI WA BIASHARA NA MAENDELEO YA KIUCHUMI


Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Pius Stephen Chaya, ametoa mwito kwa watafiti kuelekeza nguvu katika tafiti zinazojibu changamoto halisi za wananchi, hususan namna ya kuongeza ajira, uzalishaji, kupanua masoko na kuboresha maisha ya watu.

Ameyasema hayo wakati wa kufungua Kongamano la Tano la Kimataifa la Usimamizi wa Biashara na Maendeleo ya Kiuchumi la Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), lililofanyika jijini Dodoma.

Dkt. Chaya amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kudumu kati ya vyuo, taasisi za utafiti, Serikali na sekta binafsi ili kuhakikisha matokeo ya tafiti yanawafikia watunga sera na wafanyabiashara na kutumika katika kuboresha maamuzi na utekelezaji wa mipango ya maendeleo.

Ametoa mwito kwa TIA, vyuo vikuu, taasisi za utafiti, Serikali na sekta binafsi kuimarisha ushirikiano katika kujenga uchumi unaotegemea maarifa, ubunifu na tija, akisisitiza kuwa Dira 2050 haitafikiwa kwa mipango pekee, bali kupitia maamuzi sahihi, uwekezaji wenye tija na utekelezaji wenye matokeo.

Ili kuhakikisha tafiti zinazofanyika zinachangia moja kwa moja katika utekelezaji wa Dira 2050, Dkt. Chaya amesisitiza umuhimu wa kuzingatia maeneo matano ya kimkakati ambayo ni usimamizi na urahisishaji wa biashara; uwekezaji na ushindani; teknolojia na ubunifu; ajira na ujuzi; pamoja na uzalishaji na masoko.

Amesisitiza umuhimu wa kutumia teknolojia, mifumo ya kidijitali na Akili Unde (AI) kuongeza tija na kuboresha usimamizi wa biashara, pamoja na kuoanisha elimu na mafunzo na mahitaji halisi ya soko la ajira, hususan kwa vijana.
Amtoa mwito kwa washiriki wa kongamano hilo baada ya kongamano hilo, waandae na kuiwasilisha Serikalini nyaraka ya mapendekezo ya kisera (Policy Brief) yenye mapendekezo mahsusi, yanayotekelezeka na yanayopimika, kwa ajili ya kusaidia kuboresha sera na mipango ya Taifa.