Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji

Habari

PROF. MKUMBO AHIMIZA MAPENDEKEZO YA RIPOTI YA HALI YA UCHUMI KUTUMIKA KUBORESHA MAENDELEO YA NCHI


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais. Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, ameelekeza kuwa matokeo na mapendekezo ya Ripoti ya Hali ya Uchumi Tanzania (Tanzania Economic Update), Toleo la Septemba 2026 yatumike katika kuboresha sera, mipango na utekelezaji wa hatua za maendeleo, hususan katika kuongeza ajira zenye tija na kuboresha kipato cha Watanzania.

Prof. Mkumbo ameyasema hayo leo, Oktoba 2, 2026, wakati akizindua rasmi Ripoti ya Hali ya Uchumi Tanzania, yenye kaulimbiu Kufanya Ajira kuwa Zenye Kuleta Tija (Tanzania Economic Update : Making Jobs Work) katika hafla iliyofanyika Dar es Salaam.

Ripoti hiyo ya Benki ya Dunia inaangazia namna Tanzania inavyoweza kuhakikisha ukuaji wa uchumi unazalisha ajira bora, zenye tija na zinazoboresha maisha ya wananchi. Amesema Tanzania haipaswi kupima maendeleo kwa kuangalia idadi ya sera, mipango, programu na bajeti zilizotekelezwa pekee, bali inapaswa kuangalia matokeo yanayopatikana, ikiwemo ongezeko la uzalishaji, ajira zenye tija, kipato, ushindani wa biashara na uboreshaji wa maisha ya wananchi.

“Ni lazima tuanze kupima maendeleo kwa matokeo, si michakato pekee. Tunapaswa kujiuliza kama uwekezaji tunaoufanya unaongeza uzalishaji, kama biashara zinaongezeka na kuwa na ushindani, kama Watanzania wanapata ujuzi unaotambuliwa na kama kipato na fursa za kiuchumi vinaongezeka,” amesema Prof. Mkumbo.