Habari
DKT. CHAYA AFUNGUA RASMI MASHINDANO YA 56 YA SHIMMUTA YANAYOENDELEA MKOANI MOROGORO
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji,Dkt. Pius Chaya, ameyataka mashirika ya umma, taasisi za Serikali na kampuni binafsi kuhakikisha kushiriki kikamilifu Mashindano ya SHIMMUTA kila mwaka kwa kuyajumuisha katika mipango na bajeti zao za mwaka.
Dkt. Chaya ametoa kauli hIyo leo, Novemba 21, 2026, wakati akifunga rasmi Mashindano ya 56 ya SHIMMUTA yaliyofanyika katika Uwanja wa Jamhuri, mkoani Morogoro, kuanzia Novemba 6 hadi 21, 2026, yakishirikisha jumla ya taasisi 96.
Aidha, Dkt. Chaya amesisitiza umuhimu wa michezo katika kuimarisha afya ya mwili na akili, kujenga nidhamu, ushirikiano na mshikamano miongoni mwa watumishi, akibainisha kuwa watumishi wenye afya njema wana mchango mkubwa katika kuongeza tija na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Ameongeza kuwa michezo haipaswi kuishia kwenye mashindano pekee, bali iwe utamaduni endelevu katika maeneo ya kazi, huku akizitaka taasisi kuhakikisha zinaanzisha mifumo ya mazoezi na ustawi wa watumishi mwaka mzima.
Vilevile, amezitaka taasisi za umma kuongeza ufanisi, tija na mchango wake katika uchumi wa Taifa, sambamba na kuunga mkono utekelezaji wa Dira 2050.
Katika hatua nyingine, ameuagiza uongozi wa SHIMMUTA kuanza maandalizi ya mashindano ya SHIMMUTA kwa mwaka 2027 yafanyike jijini Arusha kabla ya kuanza AFCON 2027, ili kuongeza kasi ya maandalizi ya Tanzania kuwa mwenyeji mwenza wa mashindano hayo.
Dkt. Chaya pia amewapongeza waandaaji, washiriki, wadhamini na wadau wote waliofanikisha mashindano hayo, akisisitiza kuwa kaulimbiu ya mwaka huu, “SHIMMUTA 2026: Michezo Ituunganishe Kuelekea AFCON,” ni wito wa kuimarisha umoja na mshikamano kupitia michezo.
