Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji

Habari

DKT. CHAYA APONGEZA UWEKEZAJI WA DOLA MILIONI 2.6 KATIKA KIWANDA CHA CHAI NJOMBE


Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Dkt. Pius Chaya, ameipongeza Kampuni ya Browns Plantations Tanzania kwa uwekezaji wa Dola za Marekani milioni 2.6 katika upanuzi na maboresho ya kiwanda chake cha kusindika chai cha Kabambe mkoani Njombe. 

Dkt. Chaya ametoa pongezi hizo wakati wa ziara yake ya kikazi kiwandani hapo, alipokwenda hali ya uwekezaji katika mkoa huo.

Dkt. Chaya amesema upanuzi wa kiwanda hicho utaongeza uwezo wa kupokea na kusindika majani mabichi ya chai kutoka kwa wakulima, hivyo kuwapa uhakika wa soko la mazao yao na kuongeza hamasa ya kuendeleza kilimo cha chai. Ameeleza kuwa uwekezaji huo una umuhimu katika kukuza shughuli za uzalishaji na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wakulima wanaojihusisha na zao hilo.

“Sisi kama Serikali tunatoa wito kwa wawekezaji wengine, waige mfano wa Browns Plantation Ltd, kwa sababu wananchi wetu wa Njombe na Mkoa wa Iringa kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakitegemea kilimo cha chai, hatutaki kuona wananchi wetu, wakihangaika wapi wauze chai.”

Kwa upande wake Bi.Rebeka Mamuya meneja wa kiwanda hicho amesema upanuzi wa kiwanda hicho unatarajiwa kukamilika mwaka 2027 na wanatarajia kuchakata majani mabichi ya chai kutoka tani 40 hadi tani 80 kwa siku.

Bi. Rebeka amebainisha kuwa, katika kuimarisha uzalishaji wa chai, kampuni inashirikiana na wakulima wadogo 3,705 kupitia Kampuni ya Kuhudumia Wakulima Wadogo Njombe (NOSC), kwa lengo la kuwawezesha kuongeza uzalishaji, kushiriki katika mnyororo wa thamani wa zao la chai na kupata soko la uhakika kupitia kiwanda hicho.

Browns Plantations Tanzania Limited inajihusisha zaidi na uzalishaji wa chai nyeusi aina ya CTC (Crush, Tear and Curl), inayosambazwa katika masoko ya ndani na nje ya nchi. Kampuni hiyo inakadiriwa kuchangia zaidi ya asilimia 75 ya uzalishaji wa chai nchini, huku uzalishaji wake wa mwaka ukitarajiwa kufikia takribani kilo milioni 12.1.