Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji

Habari

DKT. CHAYA AITAKA DSE KUENDELEA KUTOA ELIMU YA FURSA ZA UWEKEZAJI


Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mheshimiwa. Dkt. Pius Chaya, tarehe 31 Agosti, 2026 amekutana na Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Bw. Peter Nalitolela, aliyemtembelea ofisini kwake kwa ajili ya kutoa salamu na kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya OR-MU na DSE.

Katika mazungumzo hayo, Mhe. Dkt. Chaya ameitaka DSE kuongeza wigo wa kuangazia fursa za uwekezaji, hususan katika uwekezaji wa umma, pamoja na kusaidia mashirika na kampuni zinazofanya biashara kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa mitaji.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika uwekezaji, kwa kuzingatia malengo ya Dira 2050, ambayo inalenga sekta binafsi kuchangia asilimia 70 la Pato la Taifa kupitia uwekezaji na biashara.

Mhe. Dkt. Chaya pia ameitaka DSE kutoa elimu zaidi kwa wawekezaji, hususan wawekezaji wa ndani, kuhusu fursa zinazopatikana katika Soko la Hisa, maeneo yenye fursa za uwekezaji na namna ya kutumia masoko ya mitaji kupata mitaji. Pia ameshauri DSE kuangalia namna ya kuimarisha ushirikiano wake na TISEZA katika kukuza uwekezaji nchini.

Kwa upande wake, Bw. Nalitolela amesema DSE imepokea ushauri uliotolewa na Naibu Waziri na kwamba itaufanyia kazi kwa lengo la kuendelea kuimarisha mchango wa Soko la Hisa katika kukuza uwekezaji na maendeleo ya uchumi nchini.